Mwenyekiti wa tawi la CCM Moscow Dr. Salim Mfungahema pamoja na uongozi wote wa tawi kwa pamoja wameunga mkono kauli ya mwenyekiti wa CCM taifa Dr. Jakaya Kikwete aliyoitoa juzi wakati akifunga mafunzo kwa watendani na viongozi wa wilaya na mikoa wa Chama Cha Mapinduzi nchi nzima yaliyomalizika huko Dodoma juzi tarehe 24 oktoba 2013.
Mwenyekiti wa chama taifa Dr. Jakaya Kikwete ameonesha wasiwasi wake juu ya mafanikio ya chama katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani (2014) na katika uchaguzi mkuu ujao ( mwaka 2015) kutokana na vitendo vya baadhi ya viongozi wa chama kutokuwa na maadili mema . Katika hotuba yake, Dr.Kikwete alisema, nukuu: “Kama hatutabadilika katika suala la rushwa, mwaka 2015 tutakuwa na wakati mgumu sana, na kama mwaka huo tutafanikiwa kuishika serikali, basi mwaka 2020 hatutarudi tena madarakani…”.
“… Najua rushwa ipo na mnaendelea kupokea sh laki mbili za ‘airtime’ (muda wa mawasiliano), ndugu zangu hatutafika, ama wengine watavuka na wengine kukwama,” alisema.” Mwisho wa kunukuu.
Tawi linaunga mkono kauli hiyo kutokana na hali halisi kwamba katika chaguzi zijazo, chama kitakuwa na wakati mgumu sana ili kushinda. Ni lazima viongozi wabadilike kwa manufaa ya wanachama wao na watanzania wote. Mwenyekiti wa chama taifa kaonesha kusikitishwa na hali ilipofikia ya baadhi ya viongozi kufikia hatua ya kupokea rushwa kwa njia ya simu. Viongozi wa aina hiyo ni lazima waachie ngazi na wawajibishwe.
Hata katika utendaji, viongozi wa vyama vya upinzani kwa sasa wanafanya kila wawezavyo kukaa karibu na wananchi na kusikiliza shida kero zao mara kwa mara. Wakati viongoziw walio wengi kwa upande wa chama chetu hawafanyi vitu kama hivyo kwa kasi ambayo ingewavunja nguvu wapinzani. Lazima tujue kuwa kila nafasi inayopatikana, wapinzani wanaitumia kwa nguvu zote ili kujiimarisha hasa kwaajili ya chaguzi zijazo.
Kiongozi anapoonekana si muadilifu, basi ni lazima kuachia ngazi na chama kumwajibisha kwa manufaa ya chama na kwa kufanya hivyo tutaweza kujenga imani ya wanachama wetu. Kazi ya kujenga imani kwa wanachama ambao wamechoshwa na matendo maovu ya baadhi ya viongozi ndani ya chama ni kazi ngumu sana. Kwani ukishapoteza imani ya wanachama juhudi za kurejesha imani yao kwa chama tena zinagharimu muda na rasilimali maradufu ili angalau kuweza kurudisha imani ya wachache kati ya wengi ambao watakuwa wamepoteza imani kwa chama.
![]() |
| Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya watendaji na viongozi wa CCM ngazi za wilaya na mikoa hapa nchini, mjini Dodoma. |
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI.
Imetolewa na Katibu wa Tawi
Hassan H. Kapilima



No comments:
Post a Comment